Mbaroni kwa kusafirisha dawa za kulevya

0
219

Jeshi la Polisi Mkoani Arusha linamshikilia mkazi mmoja wa Arusha mjini akiwa anasafirisha madawa ya kulevya aina ya mirungi kwa kutumia gari la kubeba mafuta.

Kamanda wa Polisi mkoani humo Justine Masejo amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa kupitia operesheni iliyokuwa ikiongozwa Mkuu wa upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha.

Kamanda Masejo amesema kuwa tarehe 10.09.2022 asubuhi katika mtaa wa Kikwe uliopo katika kata ya Kikwe wilayani Arumeru, Jeshi hilo la Polisi lilifanikiwa kumkamata mtu mmoja aitwaye Allen Wilbard Kasamu (49) dereva na mkazi wa Suye Jijini Arusha akiwa anasafirisha madawa ya kulevya yadhaniwayo kuwa ni mirungi yenye uzito wa zaidi ya robo tani ambao ni kilo 390.75kg.

Amebainisha  kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa anasafirisha madawa hayo ya kulevya kwa kutumia gari aina ya Mitsubish Canter – Tanker ambalo ni maalumu kwa ajili ya kubeba mafuta ambapo alitumia mbinu za kupakia ndani ya tenki la mafuta ili asijulikane.

Hata hivyo Kamanda  Masejo amesema kuwa hadi hivi sasa jeshi la Polisi mkoani humo  bado linaendelea na upelelezi hivyo upelelezi utakapokamilika jalada litapelekwa ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya kutolewa maamuzi.

Ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa Jeshi la polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.