Mbaroni kwa kujifanya Dkt. Abbasi

0
164

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa wawili kwa makosa ya kimtandao kufuatia msako unaofanywa na kikosi maalum cha kupambana na makosa hayo.

Miongoni mwa watuhumiwa hao ni Innocent Chengula ( 23), mkazi wa Kigogo, Dar es Salaam ambaye amekamatwa kwa tuhuma za kujitambulisha kuwa yeye ni Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu wa wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mtuhumiwa huyo amekuwa akijitambulisha kwa jina hilo wakati akiwasiliana na watu mbalimbali, na amekuwa akiweka picha na majina ya Dkt. Hassan Abbasi kwenye kurasa zake za mitandao yake ya kijamii huku akituma jumbe kwa watu akiwaomba msaada.

Polisi wamesema miongoni mwa jumbe hizo zinasomeka “kaka naomba niazime shilingi milioni 3 alhamisi nitakurudishia.” na nyingine “kaka nina mtoto wangu naomba umpatie kazi apo kwako yeye amesomea bachelor of commerce in accounting”.

Tazarn Mwambengo (27) mkazi wa Ukonga, Dar es Salaam, yeye anatuhumiwa kusambaza taarifa za uongo kuhusu kifo cha Dkt. Harrison Mwakyembe kupitia chaneli ya televisheni ya mtandaoni, jambo ambalo si la kweli.

Katika chaneli hiyo mtuhumiwa huyo aliandika “Breaking News, huzuni yatanda mazishi ya Mwakyembe” Taarifa ambazo ziliibua taharuki kwa wananchi hasa kwa Dkt. Mwakyembe mwenyewe na familia yake.