Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberate Mulamula amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Raychelle Omamo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya marasi wa nchi hizo ya kukutana ili kuondoa vikwazo vya kibiashara baina ya nchi hizo.
Mawaziri hao pia wamekutana na kufanya mazungumzo na wafanyiashara Wanawake wa Tanzania, kwa lengo la kuwatia moyo na kuwaonesha fursa za kibiashara zilizopo nchini kenya.
Wakati wa mazungumzo hayo yaliyofanyika mkoani Dar es salaam, Balozi Mulamula amemhakikishia Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Kenya kuwa Tanzania ipo tayari kuendelea kutoa fursa kwa Wafanyabiashara wa nchi hiyo kuendelea kuwekeza hapa nchini.
Kwa upande wake Waziri Omamo amesema Kenya itaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia biashara, ili Watanzania wengi waendelee kuwekeza nchini humo.
Tanzania na Kenya zimekubaliana kufungua milango ya mahusiano ya kibiashara, na kuondoa vikwazo vilivyokuwa vinakwamisha biashara baina ya nchi hizo mbili.