Mawakili nchini wasisitizwa kuzingatia maadili

0
225

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma amewataka mawakili nchini kuzingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu yao, ili kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa dhidi yao.

Jaji Mkuu ametoa kauli hiyo mkoani Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kuwaapisha na kuwakubali mawakili wapya 314.

Amesema katika kipindi hiki ambacho dunia yote ni kijiji, hakuna nafasi kwa Mawakili wasio na maadili na sifa, hivyo ni vema wakazingatia jambo hilo.

Jaji Mkuu wa Tanzania amewataka mawakili nchini kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapoona kuna mawakili miongoni mwao wasio na maadili ambao wamekuwa wakichafua taaluma yao, ili wachukuliwe hatua stahiki.

Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliezer Feleshi amewataka mawakili hao wapya kutambua kuwa uwakili ni taaluma adhimu, hivyo wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria za nchi.

Pia amewataka Mawakili hao wapya kufuata na kuheshimu taratibu za kimahakama, na waache kuwatoza wateja wao kiwango kikubwa cha fedha tofauti na kile kilichoainishwa katika sheria zilizopo.