Mawakili Kanda ya Shinyanga wafundwa

0
210

Mawakili wa serikali na wale wa kujitegemea wametakiwa kuwa na hofu ya Mungu na kuzingatia maadili wanapotekeleza majukumu yao ili kuwezesha wananchi kupata haki zao kwa wakati.

Rai hiyo imetolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Athuman Matuma wakati wa kikao kazi cha mawakili na wadau wa mahakama wa kanda hiyo.

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo aliwataka mawakili wote kuzingatia sheria na kuheshimu viapo vyao ili wasiwe chanzo cha wananchi kutopata haki zao za msingi kwa wakati.

“Asitokee wakili katika kanda yetu ya Shinyanga atakayekuwa chanzo cha uvunjaji wa maadili kwa kutotenda haki kwa mwananchi,” amesema Jaji Mtuma.

Pamoja na mambo mengine Jaji Mtuma amewataka wadau wa sheria waliohudhuria katika kikao hicho kutoshiriki vitendo vya rushwa ambavyo kimsingi ni chanzo cha ukosefu wa haki kwa wananchi.

Baadhi ya washikri walioshiriki kikao hicho wamesema mkutano huo utasaidia kuleta tija na matokeo chanya katika kufikia lengo la mahakama la utoaji haki kwa wakati.