Matukio 10 makubwa Siku 100 za Rais Samia madarakani

0
222

Saa 2,400 sawa na siku 100 zimetimia tangu Samia Suluhu Hassan alipoapishwa kuwa Rais wa Tanzania wa awamu ya sita, shughuli iliyofanyika Machi 19, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Wakati watu wengi hufurahi na kusherehekea wanapoapishwa, haikua hivyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwani aliapishwa kushika wadhifa huo kufuatia kifocha Rais Dkt. John Pombe Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.

Baada ya kutwaa ofisi, Rais Samia amepitia au amefanya mambo mengi makubwa, na hapa tutaelezea mambo makubwa kumi aliyopitia au kufanya tangu aliposema “Eeh Mwenyenzi Mungu nisaidie.”

  1. Msiba wa Dkt. Magufuli
    Kama ilivyoelezwa hapo juu, Rais Samia Suluhu Hassan aliapishwa siku mbili baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.

Tukio hilo lilikuwa ni la kwanza Tanzania kwa Rais aliye madarakani kufariki, hivyo Taifa lilikuwa mithili ya mtoto aliyefiwa na baba, asiyejua maisha yake yatakwendaje. Msiba huo ulikuwa ni jambo la kwanza ambalo Rais Samia alipambana nalo kwa kulifariji na kuliunganisha Taifa. Lakini pia alitumia jukwaa hilo kuwatoa hofu wale wote waliokuwa na wasiwasi kama angeweza kuiongoza Tanzania.

“… aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye maumbile yake ni mwanamke,” ni kauli ya Rais Samia ambayo iliwafanya waombolezaji kushangilia na kutabasamu katilati ya majonzi ya msiba.

Mwili wa Dkt. Magufuli ulizikwa nyumbani kwake Chato mkoani Geita Machi 26, 2021, shughuli ambayo iliongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

2. Hotuba bungeni
Baada ya kutwaa madaraka, Rais alihitaji kutoa mwelekeo wa serikali yake ya awamu ya sita, na alifanya hivyo kupitia hotuba yake aliyoitoa bungeni Aprili 22, 2021.

Rais alitumia nafasi hiyo kueleza mambo kadha wa kadha ambayo serikali yake itayafanya ikiwa ni pamoja kudumisha mazuri ya awamu zilizopita, kuendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya.

Akisimama bungeni hapo kama Rais kwa mara kwanza alieleza kuwa serikali itahakikisha uchumi unakua zaidi, kuendelezwa kwa vita dhidi ya rushwa, kudhibiti ugonjwa wa Corona, kuboresha huduma za afya, kuimarisha demokrasia na ushirikiano wa kikanda na kimataifa. Pia aliwaonya waliokuwa wakizusha kuhusu chanzo cha kifo cha Dkt. Magufuli ambaye alifariki kwa tatizo la moyo.

3. Kukutana na Makundi Maalum
Kama ambavyo ilikuwa kwa watangulizi wake, Rais Samia alianza kwa kukutana na makundi maalum ambapo hadi sasa ameshakutana na wazee (Dar es Salaam), viongozi wa dini (Dodoma), Wanawake (Dodoma) na Vijana (Mwanza).

Rais Samia ametumia mikutano yake na makundi hayo kuzungumza na Taifa kuhusu masuala yanayohusu kundi husika. Mfano, alipokutana na wazee alitumia nafasi hiyo kueleza masikitiko yake kuhusu kukua kwa utamaduni usio wa Kitanzania ambao vijana hawawatunzi wazee wao. Akisema licha ya kwamba serikali itajenga makazi ya wazee, lakini tamanio lake ni kuona wazee wanaishi na ndugu zao, badala ya kupelekwa kwenye makazi hayo ambayo inaonekana kama wametelekezwa.

Kwenye mikutano hiyo pia alieleza nafasi ya viongozi wa dini kuhakikisha amani na usalama vinaendelea nchini, umuhimu wa wanawake kujiamani na kujikwamua kiuchumia na vijana kutumia fursa zilizopo kujiajiri na wale wanaopata nafasi za ajira kuzitumia na kuonesha kuwa vijana wanaweza kuaminiwa.

4. Panga/pangua viongozi
Kwa siku 100 alizokaa madarakani Rais amefanya uteuzi wa viongozi wapya, ametengua uteuzi wa wengine na wengine wakihamishwa vituo vya kazi, yote hii ikiwa ni kuhakikisha anapanga safu yake na Kazi inaendelea.

Miongoni mwa teuzi alizosafanya na uteuzi wa mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, majajji wa mahakama ya rufani na mahakama kuu viongozi wa taasisi mbalimbali za serikali na wenyeviti wa bodi za taasisi za serikali.

Wito wake mkuu kwa viongozi wote aliowateua ni kuwatumikia wananchi na kwamba wasianze kunyanyua mabega. Aliwafahamisha kuwa wapo watu wengi wanaoweza kushika nyadhifa zao, hivyo hatosita kutengua uteuzi wa yeyote muda wowote. Katika teuzi zake, Rais ametoa nafasi kubwa kwa vijana na pia ameteua mwanachama wa chama cha siasa cha upinzani, Queen Sendiga kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ikiwa ni uthibitisho wa kauli yake hatojali itikadi, rangi, kabila au vyama katika uteuzi wake.

5. Ugonjwa wa Corona
UVIKO-19 ni janga ambalo linaendelea kuitesa dunia ambapo sasa tishio kubwa ni wimbi la tatu la maambukizo ambalo limeendelea kusambaa katika nchi mbalimbali duniani.

Baada ya kutwaa madaraka, Rais alisema kuwa Tanzania haiwezi kujitenga kama kisiwa, kwa kuamini kwamba madhara yanayoikumba nchi nyingine hayawezi kufika Tanzania. Rais alianza kwa kuunda kamati ya wataalamu kumshauri kuhusu hatua za kuchukua kukabiliana na ugonjwa huo.

Kamati iliwasilisha mapendekezo kwake, na miongoni mwa iliyoshauri ni serikali kuruhusu chanjo ya UVIKO-19 nchini, lakini uamuzi wa kuchomwa au kutochomwa ubaki kwa mwananchi mwenyewe. Kamati pia ilishauri wananchi waendelee kuchukua hatua kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

Hatua alizochukua Rais kukabiliana na ugonjwa huo, hasa yeye mwenyewe kuwa mfano wa uvaaji barakoa zimepongezwa na wengi kwani zitasaidia kupunguza maambukizi mapya.

6. Maelekezo kwa taasisi
Ndani ya siku 100 za uongozi wake, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo kwa wizara na taasisi mbalimbali za serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) lengo likiwa ni kuboresha maisha ya wananchi. Mfano, akiwa Mwanza aliiagiza CCM kukarabati viwanja inavyomiliki ili viweze kutumiwa na vijana.

Pia aliwaagiza viongozi wa mikoa kihakikisha wanatatua kero za wananchi na kwamba akiwa ziarani kwenye mikoa husika, na akaona bango la kero iliyotakiwa kutatuliwa kwenye ngazi ya mkoa/wilaya, basi viongozi husika wataondolewa.

7. Bomba la mafuta & SGR
Baada ya kutwaa kijiti cha uongozi, moja ya ahadi alizotoa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuendeleza miradi ya kimkakati iliyoasisiwa na serikali ya awamu ya Tanzania ikiwemo mradi wa kufua umeme wa maji wa Nyerere (JNHPP), ujenzi wa madaraja na miundombinu mingine.

Kuthibitisha kauli yake, Mei 20 alishuhudia utiaji saini wa mkataba hodhi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki litakalojengwa kuanzia Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Mafuta Ghafi ya Afrika Mashariki (EACOP).

Aidha, Juni 14 aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kipande cha tano cha SGR kutoka Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga chenye urefu wa 341km ambacho ujenzi wake utagharimu shilingi trilioni 3.1.

8. Ziara nje ya nchi
Katika 100 zake madarakani, Rais Samia Suluhu Hassan ametembelea nchi tatu za Afrika, ziara zote zikiwa na madhumuni tofauti.

Aprili 11 mwaka huu, Rais Samia alifanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi ambapo alikwenda nchini Uganda
ambapo yeye na mwenyeji wake walishuhudia utiaji saini wa mikataba ya utekelezaji wa mradi ujenzi wa bomba mafuta ghafi la Afrika Mashariki (East Africa Crude Oil Pipeline – EACOP) kati ya Serikali na kampuni za uwekezaji uliofanyika katika Ikulu ya Entebbe nchini Uganda.

Mei 12 alirudi tena Uganda kuhudhuria kuapishwa kwa Rais Yoweri Museveni. Akiwa Uganda alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde.

Safari yake ya tatu, lakini kwenye nchi ya pili ilikuwa nchini Kenya ambapo alifanya ziara ya siku mbili, Mei 4 na 5 ambapo alifanya mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta, aliutubia jukwaa la Wafanyabiashara wa Kenya na kuhutubia Bunge la Kenya.

Safari yake ya tatu ilikuwa Juni 22 ambapo alikwenda nchini Msumbiji kuhudhuria Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Juni 23, 2021.

9. Kupandisha madaraja
Baada ya watumishi wa umma kukaa kwa miaka mitano bila kupandishwa madaraja na mishahara, Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kufanya hivyo, na tayari baadhi ya watumishi wa umma wameshaonja neema hiyo.

Tayari watumishi 70,437 wamepandishwa madaraja, na serikali imetengza shilingi bilioni 300 kuhakikisha kuwa kila anayepanda analipwa stahiki zake.

10 . Bajeti
Juni 22 Bunge la Tanzania lilipitisha bajeti kuu ya serikali kwa mwaka 2021/22 ya shilingili trilioni 36.66, ikiwa ni bajeti ya kwanza chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Bajeti hiyo imepokelewa kwa mikono miwili kwa kutoa ahueni kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kupunguza faini za bodaboda kutoka shilingi 30,000 hadi 10,000, kupunguza kodi ya shayiri inayozalishwa nchini, kufuta tozo iliyokuwa inatozwa na bodi ya mikopo kwa kutunza deni la mhitimu.

Aidha, bajeti hiyo imeelezwa kuwa itakuwa kichocheo kwa ukuaji wa viwanda vya ndani, ukuaji wa sekta ya kilimo pamoja na kuongeza motisha kwa watumishi wa umma katika kuwatumikia wananchi.