Matokea ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi yatangazwa

0
1961

Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA ) limetangaza matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE ) uliofanyika tarehe Tano  na Sita mwezi Septemba mwaka huu ambapo jumla ya watahiniwa 733, 103 kati ya 943,318 wamefaulu mtihani huo.

Katibu Mtendaji wa NECTA Dkt Charles Msonde amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuwa watahiniwa hao waliofaulu wamepata alama 100 na zaidi kati ya alama 250 zinazohitajika  na kwamba idadi hiyo ya waliofaulu ni sawa na asilimia 77.72.

Kwa mujibu wa Dkt Msonde, mwaka 2017 watahiniwa walifaulu kwa asilimia 72.76, hivyo kuna ongezeko la ufaulu kwa asilimia 4.96.

Kwa upande wa ufaulu kimasomo, Dkt Msonde amesema kuwa takwimu za matokeo zinaonesha kuwa katika masomo ya kiingereza, maarifa ya jamii, hisabati na sayansi ufaulu umepanda kwa kati ya asilimia 4.03 na 11.92 ikilinganishwa na mwaka 2017 huku kwa somo la kiswahili ufaulu wake ukishuka kwa asilimia 1.44 ikilinganishwa na mwaka 2017.

Katibu Mtendaji huyo wa NECTA Dkt Charles Msonde ameongeza kuwa watahiniwa wamefaulu zaidi katika somo la Kiswahili na katika somo la kiingereza wamefaulu kwa kiwango cha chini zaidi.

Amezitaja shule kumi bora zilizofanya vizuri kitaifa zenye idadi ya watahiniwa zaidi ya arobaini kuwa ni Raskazone ya mkoani Tanga, Nyamuge ya mkoani Mwanza, Twibhoki ya mkoani Mara, Kwema Modern na Rocken Hill za mkoani Shinyanga, St Anne Marie ya mkoani Dar es salaam, Jkibira, St. Achileus Kiwanuka, St. Severine na Rweikiza zote za mkoani Kagera.

Shule Kumi ambazo hazikufanya vizuri kitaifa ni Mangika ya mkoani Tanga, Mwazizi ya mkoani Tabora, Isebanda ya mkoani Simiyu, Malagano ya mkoani Tabora, Magana ya mkoani Mara, Kododo ya mkoani Morogoro, Mtindili ya mkoani Tanga, Lumalu ya mkoani Ruvuma, Chidete ya mkoani Dodoma na Mavului ya mkoani Tanga.