Matende, mabusha, minyoo, trakoma mwisho 2030

0
166

Serikali imetangaza mikakati kabambe kuhakikisha magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele yanatokomezwa hadi kufikia mwaka 2030.

Magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele ni pamoja na usubi, kichocho, minyoo ya tumbo, trakoma/vikope, matende na mabusha yameathiri Watanzania wengi kwa sehemu kubwa na kwa miaka 10 serikali imekuwa ikipambana nayo.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Taifa wa Kuratibu Magonjwa hayo Wizara ya Afya, Dkt. George Kabona, wakati akizungumzia kilele cha maadhimisho ya magonjwa hayo yaliyoanza tarehe 24 mwezi huu na yanatarajiwa kufikia kilele chake siku ya Jumapili katika viwanja vya Nyerere Square mkoani Dodoma.

Amesema miongoni mwa magonjwa hayo ugonjwa wa kichocho umeonekana kuathiri zaidi watu wengi kulinganisha na magonjwa mengine.

“Madhara yake si kiafya tu, yanasababisha unyanyapaa kwa jamii na katika mifumo ya kutolea afya hayapewi kipaumbele kiasi kwamba mtu akipata magonjwa haya akienda hospitali si rahisi kupewa huduma,” amesema

Amesema ili kukabiliana na magonjwa hayo, Serikali imekuwa ikitoa elimu kupitia njia mbalimbali ili wananchi waweze kujikinga na magonjwa hayo, pamoja na kutenga wiki ya kukuza uelewa wa magonjwa hayo.