Matembezi ya mshikamano yazalisha milioni 300

0
204

Wanachama wa Chama cha Mapinduzi wamefanya matembezi ya mshikamano ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa chama hicho.

Matembezi hayo yamefanyika mapema leo alfajiri, kabla ya kuanza kwa sherehe za maadhimisho, yakianzia Ikulu ndogo ya mjini Musoma na kupita katika mitaa ya mji wa Musoma na kuhitimishwa katika ofisi za Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara.

Matembezi hayo yameongozwa na Katibu wa CCM Taifa, Daniel Chongolo, huku yakizalisha kiasi cha shilingi milioni 300

Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amepongeza hatua hiyo na kusema fedha hizo zitasaidia kuzalisha kadi za kidigitali zitakazotumika kusajili wanachama wa chama hicho.

Mwenyekiti Samia amesema CCM imeimarika kiuchumi na kuweza kujitegemea Katika kuendesha mambo yake ikiwemo kampeni.

Aidha, amesema usimamizi mzuri wa Ilani ya CCM ndio umejenga imani kwa Watanzania kuendelea kukiamini chama hicho na kuendelea kutawala tangu kuanzishwa kwake

Chama Cha Mapinduzi kimetimiza miaka 45 tangu kilipoanzishwa baada ya kuungana kwa TANU na ASP ambapo kimekuwa kikiendelea kuongoza Tanzania Bara na Zanzibar hadi sasa.