Mashujaa kuendelea kukumbukwa

0
166

Tanzania imetakiwa kuendelea kuwaenzi na kuwakumbuka mashujaa waliopigania Taifa kwa njia ya kuweka alama ili kuvikumbusha vizazi vya sasa na vijavyo kuhusu mashujaa hao huku kukifanyika matamasha ya mara kwa mara kama sehemu ya kuhamasisha kuwaenzi mashujaa hao kwa vitendo.

Hayo yamesemwa na Dkt. Padri Xaver Komba alipozungumza na watalii wa ndani, wazee wa mila, machifu wa makabila ya Kusini na Malawi, waliotembelea maeneo ya kihistoria ilipoanzia Vita vya Majimaji kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma eneo la Maposeni kwa Chifu Mputa Gama.

Dkt. Komba amesisitiza na kushauri kuwa, jambo hili lifanywe na makabila yote nchini, Zambia, Malawi na kote kwenye utajiri wa historia ya Mashujaa kwani licha ya uhifadhi tu wa urithi huo wa kihistoria maeneo hayo yataongeza idadi ya vivutio vya utalii.

“Tusisubiri wageni waje kutujengea minara ya watu wao waliomwaga damu hapa kwetu, bali na sisi tuamke na kuongeza kasi ya kusimamisha minara kwenye maeneo ambayo tunaona ndipo wazee wetu damu yao ilimwagika kwaajili yetu, wao wakiona tumefanya hivyo na tunaendelea na utaratibu wetu, watakuja tu kutalii” Ameongeza Dkt Komba