Mashtaka 5 waliyosomewa vigogo wa Bohari ya Dawa (MSD)

0
511

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imewafikisha mahakamani na kuwasomea mashtaka matano aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Laurien Bwanakunu na aliyekuwa Mkurugenzi wa Lojistiki wa MSD Byekwaso Tabura.

Mashtaka hayo ni pamoja na uhujumu uchumi, utakatishaji wa fedha na matumizi mabaya ya madaraka.

Shtaka la kwanza linawahusu watuhumiwa wote wawili ambapo wanatuhumiwa kupanga njama na kutenda kosa kinyume na kifungu Namba 200 cha Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002.

Akisoma shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama ya kisutu, Richard Kabate, Wakili wa Serikali, Faraji Ngukah amesema watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kati ya Julai 1, 2016 na Juni 30, 2019.

Shtaka la pili katika kesi hiyo Namba 46 ya mwaka 2020 linawahusu watuhumiwa wote ambapo inadaiwa kuwa kati ya Julai 1, 2016 na Juni 30, 2019 watuhumiwa hao kwa pamoja walitenda kosa la kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 3.8.

Shitaka la tatu linamhusu Bwanakunu ambalo ni matumizi mabaya ya madaraka. Inadaiwa kuwa kati ya Julai 1, 2016 na Juni 30, 2019, mkurugenzi huyo wa zamani wa MSD aliongeza mishahara na posho kiasi cha shilingi bilioni 3.8 kwa watumishi wa mamlaka hiyo bila idhini ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Utumishi wa Umma.

Kosa la nne linawahusu watuhumiwa wote wawili na kwamba wameisababishia Bohari ya Dawa hasara ya shilingi milioni 85 baada ya kufanya uzembe na kutokea uharibifu wa dawa zilizokuwa zimehifadhiwa katika bohari hiyo.

Shtaka la mwisho ni utakatishaji wa shilingi bilioni 1.6 ambapo watuhumiwa wote wawili wanatuhumiwa kulitenda kati ya kipindi tajwa, kinyume na Sheria Namba 12 ya mwaka 2006 ya Utakatishaji wa Fedha na kifungu namba 200 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Kabate ameiahirisha kesi hiyo mpaka Juni 19, 2020, itakaporeje tena kwa ajili ya kutajwa.