Mashindano ya Taifa ya Baseball yaanza Dar es salaam

0
1690

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza mchezo wa Baseball uwe katika mfumo rasmi na kuchezwa katika mashindano mbalimbali ya Kitaifa nchini yakiwemo mashindano ya michezo kwa shule za msingi UMITASHUMTA na ya shule za sekondari  UMISSETA.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo jijini Dar es salaam wakati akizindua uwanja  na mashindano ya Taifa ya Baseball katika viwanja vya shule ya sekondari ya Azania.

Kwa upande wake waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison  Mwakyembe amesema kuwa wizara yake na idara zilizo chini yake kwa kushirikiana na wizara nyingine zinazohusika na Elimu, watahakikisha kufikia mwaka 2019 mchezo huo wa Baseball unarasimishwa na kuwa katika mfumo rasmi nchini.

Uwanja huo wa mashindano ya Taifa ya Baseball uliopo katika viwanja vya shule ya sekondari ya Azania, umejengwa kwa msaada wa serikali ya Japan kwa gharama ya zaidi ya Dola Elfu 80  za Kimarekani ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 180 za Kitanzania.

Mashindano hayo ya Taifa ya Baseball yanafanyika kuanzia leo Disemba Sita hadi  Tisa kwenye viwanja hivyo vya shule ya sekondari ya Azania ambapo timu 14 kutoka mikoa 11 nchini zinashiriki.

Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mkuu wa Chama Cha Baseball na Softball nchini Hellen Sima, mashindano hayo yatatumika kupata wachezaji nyota wa Timu ya Taifa ya wanaume na wanawake, watakaopeperusha bendera ya Taifa katika kampeni ya kusaka tiketi ya kufuzu michuano ya Olimpiki ya mwaka  2020 itakayofanyika nchini Japan.