Mashamba ya Zabibu, fursa ya utalii inayokua kwa kasi

0
196

Miongoni mwa sekta ya Utalii inayokua kwa kasi nchini ni uwepo wa mashamba ya Zabibu yaliyopangwa katika mfumo wa kuvutia.

Zabibu ni zao lenye upekee ambalo hulimwa mkoani Dodoma, hii ni kutokana na zao hilo kuwa rafiki na hali ya hewa ya mkoa huo, watu kutoka maeneo mbalimbali hufika kwenye mashamba hayo kujionea na kujifunza namna ya zao hilo linavyopandwa mpaka linapotoa matunda yenyewe.

Matunda yanayopatikana hayaishii kuliwa tu bali hutumika kutengeneza mvinyo (wine), kinywaji ambacho kinanywewa na watu wengi duniani.

Itakulazimu kusafiri kilometa 35 tu kutoka katikati ya jiji ya Dodoma hadi mashamba ya Zabibu yaliyopo Nkulabi yanayomilikiwa na Dane Holdings Limited ambao pia hutengeneza mvinyo katika ladha mbalimbali.

Afisa Utawala wa Kampuni hiyo Mariam Maganga , amesema wanapokea wageni kutoka ndani na nje ya nchi ambao hutembelea mashamba na kiwanda cha kuzalisha mvinyo, ili kujifunza na kuona utengenezaji wa mvinyo.

“Tunapokea wageni kutoka sehemu mbalimbali, lengo wanakuja kujionea jinsi zao la zabibu linavyokuwa shambani hadi linapobadilika na kuwa kinywaji”, amesema Mariam.