Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekumbusha kuwa hairuhusiwi huduma ya bweni kutolewa kwa wanafunzi wa elimu ya awali na darasa la kwanza hadi la nne, isipokuwa kwa kibali maalum kitakachotolewa na Kamishna wa Elimu baada ya kupokea maombi rasmi kutoka kwa mdau husika.
Taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa imeeleza kuwa shule zote ambazo zinatoa huduma ya bweni kwa madarasa yasiyoruhusiwa zinatakiwa kusitisha huduma hiyo ifikapo mwisho wa muhula wa kwanza mwaka 2023.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua hiyo ni utekelezaji wa mwongozo wa uanzishaji na usajili wa shule uliotolewa na wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwezi Novemba mwaka 2020.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kubainika baadhi ya shule zimekuwa zikipokea watoto wenye umri mdogo kuanzia darasa la awali hadi la nne, huku huduma zinazotolewa kwa wanafunzi hao zikiwanyima fursa ya kushikamana na familia na jamii zao, kujenga maadili na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya familia zao.
Kulingana na tafiti zilizopo, madhara ya muda mrefu yatokanayo na tabia ya kulaza watoto bweni katika umri mdogo ni watoto kukosa mapenzi kwa wazazi ama walezi na jamii zao na hivyo kushindwa kuwa sehemu ya familia na jamii husika.
Taarifa hiyo ya Kamishna wa Elimu pia imesema kuwa hairuhusiwi kwa shule yeyote kuwa na makambi ya kitaaluma na kuzielekeza shule kuweka mikakati thabiti ya ufundishaji na ujifunzaji kwa kuzingatia kalenda za mihula zinazotolewa mara kwa mara na Kamishna wa Elimu ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa malezi na makuzi ya mtoto yanategemea sana mchango mkubwa unaotolewa na familia kupitia wazazi ama walezi wa watoto.