Marais wa Tanzania na Burundi waahidi kuzidisha uhusiano kati ya nchi zao

0
287

Na, Emmanuel Samwel

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye yupo nchini Tanzania kwa ziara ya siku tatu yenye lengo la kuendeleza uhusiano na mashirikiano baina ya nchi mbili kupitia sekta mbalimbali za Maendeleo ikiwemo Sekta ya Biashara na Viwanda.

Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, Dodoma Rais Samia Suluhu Hassan amesema anaridhishwa na uhusiano mzuri uliopo kati Burundi na Tanzania na kusisitiza uhusiano huo kuendelezwa kwa maslahi mapana ya wananchi wa Mataifa hayo.

Aidha, Rais Samia ameipongeza Serikali ya Burundi kwa hatua mbalimbali inazochukua katika kuimarisha amani na utulivu ndani ya nchi hiyo tofauti na ilivyokuwa huko nyuma huku akiahidi mshikamano katika kuhakisha kwamba eneo la maziwa makuu na mipaka ya nchi hizo kwa ujumla linakuwa na amani na utulivu.

Kuhusu kiwanda cha Itracom cha kuzalisha mbolea jijini Dodoma Rais Samia Suluhu Hassan ameishukuru Serikali ya Burundi kumleta mwekezaji wa kiwanda hicho hivyo kuahidi ushirikiano katika ujenzi wa kiwanda hicho nakuleta tija kwa mataifa haya mawili.

Kwa upande wake Rais Ndayishimiye ameeleza kufurahishwa na mualiko wa Rais Samia ambapo amebainisha kuwa mualiko huo ni wenye tija katika masuala mbalimbali ya maendeleo hususani sekta ya Viwanda na Biashara, ikiwemo Sekta ya Mawasiliano na Nyanja ya Siasa na Usalama.

Rais Ndayishimiye amesema kuanzishwa kwa bandari kavu katika mpaka wa Tanzania na Burudani utasaidia kupunguza gharama ya kusafirisha mizigo kutoka Tanzania kwenda Burundi.

Kuhusu suala la UVIKO 19 Rais Ndayishimiye ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kutofunga mipaka yake wakati ugonjwa wa UVIKO-19 ulipopamba moto hivyo kuwafanya wananchi kuendelea na majukumu yao kama kawaida wakati mataifa mengine yakiwa yamefungia watu majumbani mwao huku akiahidi ushirikiano katika kukabiliana na ugonjwa huo kwa Ustawi wa nchi zote.

Rais Ndayishimiye atakuwa nchini kwa Ziara ya siku tatu ambapo anatarajiwa kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Mradi wa reli ya Kisasa ya SGR na Bandari Kavu ya Kwala.