Marais Magufuli, Museveni na Kenyatta wakutana

0
1643

Rais John Magufuli amekutana na Rais Yoweri Museveni na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ambao walikua jijini Arusha kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao hata hivyo umeahirishwa hadi Disemba 27 mwaka huu.

Mara baada ya kikao cha ndani kilichofanyika katika moja ya kumbi za watu mashuhuri ndani ya Kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Marais wote watatu walisafiri kwa gari moja hadi Ikulu ndogo ya Arusha.

Rais Museveni amesema kuwa mkutano huo umeahirishwa kutokana na mmoja wa wanachama wa jumuiya hiyo ambaye ni nchi ya Burundi kutohudhuria, ilihali mkataba wa jumuiya hiyo unataka maamuzi yafanywe na wanachama wote kwa pamoja.

“Tuliamua kuahirisha mkutano kwa leo kwa sababu mmoja wetu ambaye ni Burundi hakuja, tumeahirisha mkutano mpaka tarehe 27 Disemba mwaka 2018 wakati sisi wote tutakapokuwepo, kwa sababu mkataba wa Afrika Mashariki unasema mambo mawili, moja lazima tuwe na mkutano mmoja wa kawaida kila mwaka na ndio huu wa leo, lakini vile vile uamuzi wowote utakaofanyika lazima wanachama wote wawepo, kwa hiyo kama mmoja hayupo sio vizuri kuendelea, inakuwa inakwenda kinyume na mkataba”, amesema Rais Museveni.

Akiwa mkoani Arusha, Jumamosi Disemba Mosi mwaka huu, Rais Magufuli na Rais Kenyatta watafungua kituo cha huduma za pamoja mpakani katika eneo la Namanga mpakani mwa Tanzania na Kenya.