Serikali imesema ipo katika hatua za mwisho za mapitio ya Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003, na imeendelea kutekeleza afua mbalimbali zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili wazee nchini.
Kauli hiyo imetolewa wilayani Manyoni mkoani Singida na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima alipotembelea makazi ya Wazee wasiojiweza ya Sukamahela, ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani Oktoba Mosi.
Amesema wakati wa mapitio ya sera hiyo yakiendelea Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuboresha maisha ya Wazee hapa nchini, ili kuhakikisha wanapata huduma jumuishi na stahiki.
Kwa mujibu wa Dkt. Gwajima, maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani kwa mwaka huu yatafanyika katika ngazi za mikoa na kuongozwa na kauli mbiu isemayo Matumizi Sahihi ya Kidigitali kwa Ustawi wa Rika Zote.
“Sherehe za maadhimisho ya siku ya wazee itahusisha huduma mbalimbali kama vile wazee kupima shinikizo la damu, kisukari, tezi dume, huduma za msaada wa kisaikolojia na elimu kuhusu kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 pamoja na kuhamasisha wazee na wananchi kupata chanjo.” amesema Dkt. Gwajima
Akisoma taarifa ya Makazi ya Wazee Sukamahela, afisa mfawidhi wa makazi hayo Twaha Kibalula amesema wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa gari kwa ajili ya kutoa huduma kwa Wazee hao ikiwa ni pamoja na huduma za kiafya zinazopatikana kwenye hospitali za wilaya na mkoa.