Maonesho ya Julius Nyerere na John F. Kennedy yafunguliwa

0
282

Wakati Tanzania ikifanya kumbukizi ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ubalozi wa Marekani nchini umefungua maonesho maalum ya kihistoria katika Makumbusho ya Taifa yaliyopo mkoani Dar es Salaam yanayomhusisha Hayati Baba wa Taifa pamoja na Rais wa 35 wa Marekani Hayati John F. Kennedy.

Maonesho hayo yaliyopewa jina la ‘Julius Nyerere na John F. Kennedy Urafiki Uliojenga Historia’, yanaonesha picha, nyaraka na barua mbalimbali zinazoonesha mawasiliano ya viongozi hao.

Pia yanaonesha jinsi kila mmoja alivyovutiwa na mwenzake, jambo lililojidhihirisha katika uhusiano imara kati ya Marekani ni Tanzania ambao umedumu kwa zaidi ya miaka sitini.

Tayari maonesho hayo ya ‘Julius Nyerere na John F. Kennedy Urafiki Uliojenga Historia’ yamefunguliwa rasmi katika Makumbusho hayo ya Taifa na kuhudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt. Noel Lwoga ambaye amewataka Watanzania kutembelea maonesho hayo ili kujifunza historia muhimu ya Taifa la Tanzania.

Kwa upande wake Balozi wa Marekani nchini Donald Wright amesema kuwa, urafiki wa karibu uliokuwepo kati ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na John F Kennedy umekuwa msingi mkubwa wa urafiki kati ya Tanzania na Marekani mpaka sasa.

Wakati huo huo Balozi Wright amesema Marekani inafurahishwa na sera za Kidiplomasia na urafiki za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba ana matumaini ya kuwa hivi karibuni Rais Samia atatembelea Ikulu ya Marekani kama alivyofanya Hayati Mwalimu Nyerere.