Manyara yashika mkia chanjo ya UVIKO19

0
128

Mkoa wa Manyara umeshika nafasi ya mwisho kitaifa katika utoaji wa chanjo ya UVIKO – 19.

Hadi sasa mkoa wa Manyara umetoa chanjo kwa watu takribani laki tatu, idadi ambayo ni sawa na asilimia 3.7 tu ya lengo.

Akizungumza mkoani Manyara wakati wa kikao kazi cha tathmini ya utoaji chanjo ya UVIKO -19, Meneja wa mpango wa chanjo wa Taifa kutoka wizara ya Afya Dkt. Florian Tinuga amesema hadi sasa mkoa wa Ruvuma ndio unaoongoza kitaifa kwa kufikia asilimia 40 ya uchanjaji.

Lengo la kitaifa ni kufikia asilimia 70 ya kutoa chanjo dhidi ya UVIKO -19 ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi kutoka shirika lisilo la kiserikali la JHPIEGO, Maryrose Giattas amesema shirika lake litatoa zaidi ya shilingi bilioni moja kuunga mkono kampeni ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 mkoani Manyara.

Naye mkuu wa mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere amewataka watendaji mkoani humo kuhamasisha wananchi ili wajitokeza na kupata chanjo dhidi ya UVIKO -19.