Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka hiyo kwa vyombo vya habari imeelezwa kuwa hali hiyo inatokana na kusogea kwa jua la utosi na upungufu wa mvua katika maeneo mengi ya nchi.
Aidha imeelezwa pia kwamba vipindi vya jua la utosi itafikia kilele chake mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini mwa Tropiki ya Kaprikoni na hali hiyo inatarajiwa kujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini mwa Tropiki ya Kansa.
Mkoa wa Kilimanjaro uliripoti kiwango cha juu cha joto kilichofikia nyuzi joto 36.4 sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.6 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Novemba.
Vipindi vya joto kali vinatarajiwa kuendelea kujitokeza katika mwezi Novemba, 2021 na kupungua kidogo ifikapo mwezi Disemba, 2021 ambapo mtawanyiko wa mvua unatarajiwa kuongezeka sambamba na mionzi ya jua la utosi kuwa imeondoka katika maeneo ya nchi yetu.
Kutokana na hali hiyo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kutoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa za mwenendo wa hali ya hewa zinazotolewa pamoja na kutumia ushauri wa wataalamu wa kisekta ili kujiepusha na madhara yanayoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa ikiwemo joto kali.