Mamlaka Usafiri wa Anga yaipiga shule jeki

0
160

Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) imetoa msaada wa vifaa vya shule na kwa ajili ya ofisi ya walimu katika Shule ya Msingi Mnete iliyopo mkoani Mtwara kama sehemu ya kurejesha faida kwa jamii.

Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 10/-, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mwanahamisi Munkunda ameishukuru TCAA kwa kuchukua hatua ya kuleta vifaa hivyo ambavyo vitachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya elimu katika shule hiyo.

Vifaa hivyo ni madawati 20, meza na viti saba kwa ajili ya ofisi ya waalimu pamoja na mashine ya kurudufisha (photocopy machine).

“Leo ni siku njema, siyo tu kwa Shule ya Msingi Mnete bali kwa Wilaya ya Mtwara kwani vifaa hivi vitarahisisha utendaji wa waalimu pamoja na kupunguza mzigo kwa wazazi,” amesema Mwanahamisi

Mkuu huyo wa Wilaya ametoa wito kwa viongozi wanaosimamia elimu kuanzia ngazi ya kata hadi shuleni kuvitumia vifaa hivyo vizuri kwa maana ya kuvitunza ili vidumu. Pia amehimiza wadau na taasisi mbalimbali kubwa na moyo wa kusaidia jamii kama ilivyofanya TCAA.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa TCAA, Yessaya Mwakifulefule amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kutenga muda wake na kuja kushiriki tukio hili na kuahidi kuwa mamlaka itaendelea kuchangia katika maendeleo ya elimu kwani ni eneo ambalo umuhimu wake ni mtambuka kwa taifa letu.

TCAA imeendelea kuwa mdau mkubwa wa elimu kwa kutoa msaada wa namna hiyo ambapo imeshatoa msaada wa shilingi milioni 8.8/- kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Rada iliyopo mkoani Songwe, vitanda 26 kwa Shule ya Sekondari ya Azania, ilitoa pia shilingi milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 10 ya vyoo kwa Shule ya Msingi Mzambarauni ya jijini Dar es Salaam.