Mamia wamuaga Ole Nasha

0
442

Rais Samia Suluhu Hassan leo ameongoza familia, Viongozi na watu mbalimbali kuaga mwili wa aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji  William Tate Ole Nasha,  aliyefariki dunia Septemba 27 mwaka huu nyumbani kwake jijini Dodoma.
 
Miongoni mwa Viongozi walioshiriki shughuli hiyo iliyofanyika katika viwanja vya bunge jijini Dodoma ni Makamu wa Rais Dkt.  Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo.
 
Baada ya kuagwa jijini Dodoma, mwili wa Ole Nasha unatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda Ngorongoro mkoani Arusha kwa ajili ya mazishi yaliyopangwa kufanyika Oktoba 2 mwaka huu katika kijiji cha Osinoni Kakesyo.
 
Wakati wa uhai wale, Ole Nasha amewahi kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda wa takribani miaka sita, na kwa nyakati tofauti amewahi kuwa  Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, nafasi aliyohudumu hadi alipofariki dunia.