Malori yenye shehena za mizigo yaendayo nchini Burundi na Rwanda yakwama

0
329

Mwandishi Sauda Shimbo

Malori yapatayo 46 yenye shehena za mizigo yaendayo nchini Burundi na Rwanda yamekwama kwa zaidi ya wiki moja sasa katika kituo cha pamoja cha Forodha kwenye mpaka wa Holili wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.

Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya madereva wamesema licha ya kuwa na nyaraka za kuonesha mizigo yao imelipiwa mapato lakini bado uongozi wa kituo hicho umewakatalia kuwaruhusu kuendelea na safari.

Akijibu malalamiko hayo, Meneja msaidizi wa Forodha –TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Edwin Iwato amesema wameshindwa kuyaruhusu malori hayo kuendelea na safari kutokana na matatizo ya kimfumo wa kieletroniki yaliyopo katika nchi za Burundi na Rwanda ambazo zitawawezesha kupokea uthibitisho wa bidhaa walizobeba na kuandaa nyaraka kwa njia ya kielektroniki.

Kwa Mujibu wa kituo cha Forodha Holili, Malori 30 yana shehena za mbolea ambapo yanaelekea nchini Burundi huku malori 16 yanayoelekea  nchini Rwanda  yakiwa na  bidhaa tofauti tofauti.