Malipo Yote ya Wakulima wa Pamba Nchini Yatakia Kupitia Benk Kwanzia Mwaka 2020

0
397

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza kuanzia mwaka 2020, malipo yote ya wakulima wa pamba nchini yawe  yanapitia benki ambapo wakulima wataingiziwa fedha kupitia akaunti zao.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo mkoani Simiyu wakati akizungumza na Wakazi wa kijiji cha Luguru wilayani Itilima, mara baada ya kukagua ghala la pamba la Chama cha Ushirika cha Msingi cha  Maendeleo.

Amewataka Wakulima wa pamba kote nchini kufungua akaunti katika benki mbalimbali zilizopo kwenye maeneo yao ili waweze  kufanikisha jambo hilo,  na pia kuhifadhi fedha zao kwa ajili ya matumizi ya baadae.

Waziri Mkuu Majaliwa ametembelea kijiji hicho cha Luguru kwa lengo la kujionea mwenendo wa uuzaji wa zao la pamba katika Chama cha Ushirika cha Msingi cha Maendeleo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa ameelezea kukerwa na kitendo cha mamlaka ya maji wilayani Maswa, kupandisha bili ya maji kutoka shilingi elfu tano hadi Shilingi Elfu 28 na hivyo kumuagiza Mkuu wa mkoa wa Simiyu, -Anthony Mtaka akutane na wahusika hii leo.

Waziri Mkuu  Majaliwa ameeleza hayo wakati akizungumza na Wakazi wa kijiji cha Kumalija wilayani Maswa mara baada ya kutembelea ghala la pamba la Chama cha Msingi cha Kumalija.