Makamu wa Rais atembelea makumbusho ya Dkt. Livingston

0
128

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango mapema leo ametembelea Makumbusho ya kihistoria ya Dkt. David Livingstone iliopo Ujiji mkoani Kigoma.

Makamu wa Rais amejionea eneo la kihistoria alipofikia mmisionari na mpelelezi Dkt. David Livingstone mwaka 1869 ambapo pia baadae eneo hilo alifika mwandishi kutoka uingereza Henry Stanley mwaka 1871.

Akitoa maelezo kwa Makamu wa Rais muongoza watalii katika makumbusho hiyo mzee Kassim Mbingo amesema eneo la Makambusho hayo licha ya kuhifadhi historia muhimu ya ujio wa David Livingstone lakini pia imebeba historia na utamaduni wa wakazi wa mkoa wa Kigoma ikiwemo Maisha yao, vyakula , mavazi, silaha za jadi, vyombo vya kale pamoja na vyombo vya usafiri walivyotumia katika ziwa Tanganyika.

Akizungumza baada ya kutembelea makambusho hayo Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuendelea kutunza na kuhifadhi historia adhimu ya nchi yetu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye.

Amewaasa watanzania kuona umuhimu wa kufika katika maeneo ya kihistoria ya nchi ili kuweza kujifunza mengi ikiwemo utamaduni katika maeneo husika. Amewataka viongozi kuwapa motisha wanafunzi wanaofanya vizuri darasani kwenda katika vivutio vya utalii na utamaduni.

Aidha Makamu wa Rais ameagiza Wizara ya Maliasili na Utalii wakishirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kukisaidia kituo cha Makambusho ya Dkt. Livingstone ili kiweze kuendelea kutoa elimu na kuhifadhi vema historia hiyo.

Aidha amemsihi muongoza watalii katika kituo hicho mzee Kassim Mbingo kuandika kitabu kitachoweza kurithisha maarifa alionayo kwa vizazi vijavyo.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ametembelea pembezoni mwa ziwa Tanganyika na kuwasalimia wavuvi na watumiaji wa ziwa hilo ambapo amewataka watanzania wote kuendelea kulinda vyanzo vya maji pamoja na usafi katika maeneo ya vyanzo vya maji.

Amesema rasilimali ya maji ni muhimu katika maendeleo ya nchi hivyo kila mmoja aone umuhimu wa kulinda kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadae.