Makubaliano yawekwa katika kusimamia sekta ya uvuvi nchini

0
430

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amekutana na Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Rashid Ali Juma, Mjini Unguja na kumweleza kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inahakikisha miradi inayohusu wavuvi inamnufaisha mvuvi moja kwa moja.

Katika mazungumzo hayo ambayo pia yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Makame Ali Ussi, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Islam Seif Salum pamoja na watendaji wengine Naibu Waziri Ulega amesema lengo kuu la ziara yake ya siku moja Visiwani Zanzibar ni kutazama shughuli za Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu Zanzibar kupitia mradi wa Usimamizi wa Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi -SWIOFISH.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Rashid Ali Juma amesema uchafuzi wa bahari, uwepo wa maharamia na uvuvi haramu ni mambo ambayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kukabiliana nayo ili kuhifadhi bahari na kufanya sekta ya uvuvi kuwa yenye tija kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvyvi Abdalla Ulega ametoa wito kwa watendaji hao kutumia Shilingi Bilioni Tano zilizotolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya mradi wa SWIOFISH ili kuleta mapinduzi ya kweli katika sekta ya uvuvi na kuhakikisha wanafanyakazi kwa kasi kulingana na matarajio ya serikali zote mbili kwa wananchi wake.