Makatibu Wakuu wa wizara watakiwa kuzingatia sheria

0
1272

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amewataka makatibu wakuu wa wizara na makatibu tawala wa mikoa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria , kanuni, taratibu na miongozo inayotolewa na serikali kila wanapofanya maamuzi.

Akifungua kikao kazi cha siku tatu kwa viongozi hao jijini Dodoma, Balozi Kijazi amesema kuwa makatibu wakuu wa wizara na makatibu tawala wa mikoa wana jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa wanazingatia taratibu zote ili azma ya kujenga uchumi wa viwanda ifikiwe kwa wakati na kuwanufaisha Watanzania.

“Nafasi zenu ni za maamuzi, hivyo msipofanya maamuzi sahihi na kwa wakati mtakwamisha shughuli za maendeleo na huduma muhimu kwa wananchi,” amesisitiza Balozi Kijazi.

Katibu Mkuu Kiongozi amesema kuwa jukumu kubwa la washiriki wa kikao hicho ni kuhakikisha wanafanyia kazi masuala yote yatakayoazimiwa katika kikao kazi hicho kinacholenga kuongeza tija kwenye ngazi ya wizara na mikoa kwa kuzingatia azma ya serikali ya kuleta mageuzi makubwa katika nyanza zote hasa katika huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Amesema kikao kazi hicho kina umuhimu mkubwa na kitakuwa kikifanyika kila mwaka ili kuwapa fursa makatibu wakuu na makatibu tawala kubadilishana uzoefu, kubaini changamoto zilizopo na kuweka utaratibu mzuri wa kuzitatua kwa maslahi ya wanachi.

Kauli mbiu ya kikao kazi hicho kinachoshirikisha makatibu wakuu wa wizara na makatibu tawala wa mikoa ni Uongozi makini na wa pamoja unaozingatia uzalendo, uwajibikaji, utawala bora na kusimamia rasilimali zetu ni nyenzo muhimu katika kuifikisha Tanzania katika uchumi wa Kati.