Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewataka makarani wa sensa mkoani humo kuwa makini na kuacha tabia ya kwenda na vishikwambi sehemu za starehe ili kuepuka kuibiwa.
Kauli hiyo ya Babu inafuatia uwepo wa wimbi la makarani kuibiwa vishikwambi katika kipindi hiki cha sensa ya watu na makazi.
Babu ameyasema hayo wilayani Hai wakati akikagua zoezi la sensa ya watu na makazi linavyoendelea katika baadhi ya maeneo mkoani humo.
Amesema ni vema makarani wakimaliza majukumu yao kwa siku kuhakikisha vishikwambi wanaviweka katika sehemu salama na kisha waendelee na shughuli zao nyingine.
Mkuu huyo wa mkoa wa Kilimanjaro amewataka pia makarani kuongeza kasi ya kuhesabu wananchi kwani wapo wananchi wengi bado hawajafikiwa na makarani.