Makamu wa Rais ataka tija zaidi sekta ya mifugo

0
206

Serikali imesema itaendelea kuipa umuhimu Sekta ya Mifugo hapa nchini kutokana na mchango mkubwa wa sekta hiyo katika kuwainua wananchi kutoka katika lindi la umasikini kwa kutoa ajira na fursa mbalimbali.

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amesema hayo akifungua kikao kazi cha Washauri wa Mifugo wa Mikoa na wakuu wa idara za Mifugo na Uvuvi kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika ukumbi wa Kambarage Jengo la Hazina mkoani Dodoma.

Amesema sekta hiyo ni muhimu kwani huchangia usalama wa chakula, na upatikanaji wa lishe bora pamoja na malighafi katika viwanda vya kuchakata na kusindika mazao ya mifugo hususani viwanda vya nyama, ngozi na maziwa.

Amesema licha ya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa idadi ya mifugo Barani Afrika lakini bado tija ya sekta hiyo hairidhishi kutokana na kukosekana kwa huduma bora za ugani pamoja na wananchi kuendeleza utamaduni wa ufugaji wa kienyeji ambao hauzingatii ubora bali idadi kubwa ya mifugo, hali inayopelekea uwezo mdogo wa kukabiliana na magonjwa ya mifugo, upungufu wa malisho na uharibufu mkubwa wa mazingira na vyanzo vya maji.

Kutokana na hilo ameagiza kila Afisa Ugani kuwa na orodha ya wafugaji anaowahudumia, ratiba ya kuwatembelea wafugaji ili kuwashauri na kufuatilia maendeleo ya mifugo, na kupima matokeo ya huduma anazotoa.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekabidhi pikipiki 300 kwa wakuu wa mikoa wakiwakilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka ili kutumika kwa kazi za maafisa ugani katika Halmashauri 140 hapa nchini.