Makamu wa Rais ashuhudia uharibifu bonde la Mzakwe

0
138

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango leo tarehe 05 Januari 2022 ametembelea na kukagua zoezi la upandaji miti na uhifadhi wa bonde la Mzakwe lililopo mkoani Dodoma.

Akikagua uhifadhi wa bonde hilo ambalo pia ni chanzo cha maji , Makamu wa Rais ameonesha kutoridhishwa na usimamizi na ufuatiliaji wa uhifadhi wa bonde la mzakwe uliopelekea kupotea kwa miti iliopandwa hapo awali kutokana na moto uliotokea novemba mwaka 2021 pamoja na baadhi ya miti mingine kushindwa kustawi.

Makamu wa Rais amewataka viongozi wa TFS pamoja na Mkoa wa Dodoma kwa ujumla kushirikisha jamii katika uhifadhi ili wananchi watambue umuhimu wa miti hiyo pindi inapopandwa katika maeneo yao.

Aidha Makamu wa Rais amewataka Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (Tafori) kuwa na uhakika wa aina ya miti inayoweza kustawi katika bonde hilo ikiwemo miti ya asili. Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuainisha miti inayopandwa pamoja na malengo yake ili kuepusha miti inayoweza kuwa chanzo cha kupoteza maji na ile itakayoshindwa kustawi katika eneo hilo.

Makamu wa Rais amesema utekelezaji wa kampeni ya kuifanya Tanzania kuwa ya kijani ni wajibu wa kila mtanzania na kuwaagiza wakuu wa mikoa, Wilaya , Wakurugenzi , na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, watendaji wa kata na vijiji kuongoza zoezi la upandaji miti na kuisimamia kikamilifu.