Moja kati ya elimu kubwa inayotolewa kwa umma ni pamoja na umuhimu wa kufanya mazoezi kwa afya imara japokuwa sehemu moja inayosahaulika ni namna bora ya kula kwa wafanya mazoezi.
Kila mmoja anayefanya mazoezi ana lengo la kwanini anafanya mazoezi hayo na kulingana na malengo yake mlo nao huweza kubadilika badilika ili kuyafikia malengo hayo kwa kiwango kizuri.
Lakini zaidi tuangalie mfumo mzuri wa kula kwa mwanariadha ambaye kwa kupitia mazoezi anashiriki katika mashindano mbalimbali ya mazoezi kama vile Kili Marathon na Olympics ama kwa kiingereza anaitwa “athlete”.
Athlete anapaswa kuzingatia vyakula vyenye wanga, protini, mbogamboga na vimiminika ama vyakula vyenye maji maji. Miongoni mwa vyakula hivyo ni pamoja na matunda, samaki, kunde, viazi vitamu, na kutumia mafuta yatokanayo na mimea kama vile mafuta ya nazi na alizeti au mafuta ya mzaituni.
Pia wanashauriwa kupunguza matumizi ya vyakula vya sukari sana, pombe na vinywaji vyenye kafeini kama vile kahawa na vyakula vya kukaanga.
“Kadiri mafunzo yanavyoongezeka ndivyo mtu atahitaji nguvu zaidi. Wanariadha wanapaswa kuwa na uwezo wa kuzalisha nguvu hiyo,” amesema Elizabeth Devine mtaalam wa lishe aliyesajiliwa na mhadhiri wa lishe wa UMass.
Wanariadha hawa wanashauriwa pia kuhakikisha wanajenga mazoea ya kula milo kamili na kwa wakati sahihi kila mara.
Wapo wafanya mazoezi ambao kutokana na aina ya mazoezi waliyokuwa wakifanya waliishia kupata matokeo tofauti na walivyotarajia ikiwemo wale wanaotaka kujenga misuli ya miili yao lakini wanasahau kula protini ya kutosha.
Wanariadha wanaofanya vyema ni wale wanaojua kupangilia muda wao wa mazoezi na kula lakini pia aina gani ya chakula kitamfaa kabla na baada ya mazoezi.