MAJERUHI MAPOROMOKO HANANG WAFIKIA 93

0
228

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema majeruhi wa maporomoko ya matope Hanang waliopo katika hospitali zote mkoani Manyara wamefikia 93.

Dkt. Mollel amesema Wizara ya Afya imeratibu upatikanaji wa timu za madaktari kwa ajili ya kuongezea nguvu katika Hospitali za
Mkoa wa Manyara ili kutoa huduma bora na kwa haraka zaidi kwa majeruhi ambapo amebainisha kuwa madaktari hao wametoka katika Mikoa ya Arusha, Dodoma na Singida.

“Huduma zinatolewa vizuri, hakuna kilichokosekana na wagonjwa wanaendela vyema na matibabu, kila kitu kinaenda vizuri kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza jana”. -Amesema Dkt. Mollel.

Leo asubuhi Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sengida amesema kuwa idadi ya vifo vya watu waliofariki dunia kutokana na maporomoko hayo imeongezeka kutoka watu 47 hadi kufikia 49 baada ya kupatikana kwa mili mingine miwili. Maporomoko hayo yalisababishwa na mvua illyonyesha usiku wa kuamkia jana Jumapili Desemba 3, 2023 ambapo sehemu ya Mlima Hanang ilimomonyoka.