Majaliwa : TCU ongezeni udhibiti wa ubora wa vyuo

0
202

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), kuongeza udhibiti wa ubora wa vyuo vikuu, ili kuhakikisha kunakuwa na mitaala inayojibu mahitaji ya soko la ajira.

Ametoa wito huo mkoani Dar es Salaam wakati akifungua maonesho ya 17 ya elimu ya juu, sayansi na teknolojia.

Amezitaka taasisi zote za elimu ya juu nchini kuendelea kufanya mapitio ya mitaala kwa kuzingatia miongozo iliyopo, ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

“Pamoja na kusimamia taaluma Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania pia iongeze jitihada katika kusimamia masuala ya utafiti na ushauri katika vyuo vikuu ili kuvifanya viwe chachu ya maendeleo na suluhisho la changamoto mbalimbali za maendeleo ya jamii yetu na Taifa kwa ujumla.” ameagiza Waziri Mkuu

Amesema taasisi za elimu ya juu ambazo ni wazalishaji wa maarifa na ujuzi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa, hazina budi kuwa mbele ya wakati siku zote ili kuhakikisha zinabuni na kuanzisha programu mpya zinazokwenda na wakati.