Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hajaridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa miradi ya hospitali ya manispaa ya Sumbawanga pamoja na kituo cha afya cha Matanga mkoani Rukwa, ambapo tayari serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni mbili.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Sumbawanga, James Mbungano ahakikishe uchunguzi wa matumizi ya fedha za miradi hiyo unakamilika kwa wakati ili serikali iweze kuchukua hatua stahiki.
Amesema kwa mradi wa ujenzi wa hospitali ya manispaa ya Sumbawanga ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 1.5 ambao bado haujakamilika licha ya kujengwa chini ya kiwango.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema kwa kiwango hicho cha fedha walichopokea walitakiwa wawe wamekamilisha majengo matano.
Waziri Mkuu amesema mradi mwingine ni wa ujenzi wa kituo cha afya cha Matanga ambacho mpaka sasa wameshapokea shilingi milioni 500 lakini ujenzi wake bado haujakamilika.
“ Ujenzi wa vituo vya afya nchini ni shilingi milioni 400 na shilingi milioni 500 katika maeneo ya pembezoni. Hapa mlitakiwa muwe mmemaliza na kituo kianze kuhudumia wananchi.” amesema Waziri Mkuu
Mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo mwezi Novemba mwaka 2021 walipokea shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa majengo matatu ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje, maabara na kichomea taka na kwa mwezi Machi mwaka huu walipokea shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa majengo manne ambayo ni jengo la wazazi, jengo la upasuaji, jengo la kufulia na jengo la watembea kwa miguu.