Majaliwa: Hakuna mtu atakayehamishwa Loliondo

0
177

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema taarifa zinazoendelea kusambaa katika mitandaoni mbalimbali ya kijamii kuhusu uwepo wa vurugu kwenye eneo la Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha ni za upotoshaji unaofanywa na mtu ama kikundi cha watu wasioitakia nchi mambo mema.
 
Akitoa ufafanuzi wa suala la Loliondo bungeni jijini Dodoma, waziri mkuu amesema kinachoendelea katika eneo hilo kwa sasa ni uwekaji wa alama za za mipaka katika maeneo ya makazi na maeneo ya kitalii.
 
Ameliambia bunge kuwa uwekaji wa alama hizo hauhusiani na jambo la kumwondoa mtu yeyote kwenye eneo lake ama kusitisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
 
Amesema zoezi la uwekaji alama kwa ajili ya makazi ya watu na maeneo ya kitalii katika eneo hilo la Loliondo ni agizo na Rais Samia Suluhu Hassan ambalo utekelezaji wake umefuata taratibu husika ikiwa na pamoja na ushirikishwaji wa wananchi.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ameeleza kusikitishwa na tabia iliyooneshwa na baadhi ya watu ama kikundi cha watu kupandikiza chuki miongoni wa wakazi wa eneo hilo ili waone zoezi hilo la uwekaji alama ni batili na hivyo kutaka kuliharibu.
 
Amewataka wananchi wa Loliondo kuishi kwa amani na kuendelea na shughuli zao na kwamba Serikali itahakikisha inamchukulia hatua mtu ama watu wanaoendelea kutoa taarifa za upotoshaji kuhusu eneo hilo.