Wabunge wa Bunge la 12 wamemthibitisha Mbunge wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi, Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu kwa miaka mitano mingine (2020-2025) kwa kupata kura zote 350 zilizopigwa na wabunge sawa na asilimia 100.
“Kura zote zilizopigwa ni 350 hakuna iliyoharibika, hakuna kura ya hapana. Kura zote 350 zimemthibitisha Majaliwa, kwa hiyo ndugu wabunge Mheshimiwa Majaliwa amethibitishwa na Bunge hili kuwa Waziri Mkuu,” amesema Spika Ndugai.
Akizungumza baada ya kuthibitishwa, Waziri Mkuu Mteule, Kassim Majaliwa amesema amepokea uteuzi huo kwa mikono miwili na anamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameendelea kuwapa uhai wote na kushuhudia hayo, pia ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa imani kubwa aliyoionesha juu yake.
“Mheshimiwa spika naomba nitumie nafasi hii kwa dhati yangu ya moyo kumshukuru sana Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushindi mkubwa alioupata kutoka kwa Watanzania kupitia uchaguzi ambao ulifanyika hivi karibuni kwa kushinda kwa kishindo. Uchaguzi uliofanyika kwa uhuru na haki.
Jambo hili si dogo, Mwenyezi Mungu ameliongoza, namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa imani kubwa aliyonayo juu yangu na kuendelea kuniamini. Namshukuru sana na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa ushiriki wake katika kuridhia jina langu.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa jimbo la Ruangwa na mkoa wa Lindi, familia na CCM kwa ushirikiano alioupata katika kutekeleza majukumu yake katika kipindi cha miaka mitano na anaimani wataendelea kumpa ushirikiano katika kipindi cha miaka mitano mingine.
Awali, kabla ya kuthibitisha jina la Waziri Mkuu wabunge mbalimbali walizungumzia utendaji kazi wa Majaliwa ambapo Mbunge wa Tunduma, David Silinde alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumrudisha tena Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika nafasi hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba amesema Majaliwa ni kiongozi msikivu, muadilifu, mnyenyekevu, hodari, mchapakazi na ni kiongozi shupavu ambaye nafasi hiyo anaimudu na anaiweza na hakuna shaka yoyote kwamba nafasi hiyo kwamba ataitendea haki. “Kumpigia kura nyingi tunaonesha imani kwa ndugu yetu na imani na busara kwa Rais.”