Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na kwamba serikali itaendelea kuhakikisha mradi huo unajengwa kwa viwango na kukamilika kama ilivyobainishwa kwenye mkataba.
Amesema ujenzi wa reli hiyo unaendelea vizuri katika vipande vyote na kwamba serikali itahakikisha mradi huo haukwami na itakabiliana na viashiria vyote vinavyoweza kukwamisha utekelezaji wake.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa stesheni kuu ya Dodoma katika eneo la Mkonze.
Amewataka Watanzania wanaoshiriki katika ujenzi wa mradi huo wasimamie usalama wa mradi na wawe walinzi, ili ukamilike kama ilivyokusudiwa.
Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa jiji la Dodoma kuwa na mkakati wa maeneo ya uwekezaji kutokana na fursa ya ujenzi wa reli hiyo ikiwemo ujenzi wa kituo cha mabasi jirani na stesheni hiyo.
Kwa upande wake, Mkurgenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa amesema, Shirika hilo lipo kwenye mpango wa ununuzi wa vichwa vya treni na mabehewa ya mizigo.
“Hadi sasa TRC imesaini mkataba wa ununuzi wa vichwa vya treni vya umeme 19 na seti za treni 10 zenye uniti 80.” amesema Kadogosa