Majaji, mahakimu marufuku kujiunga vyama vya siasa

0
328

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma amewataka majaji na mahakimu watakaosikiliza mashauri yatakayotokana na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu kuandika hukumu hizo katika lugha nyepesi, inayoeleweka na inayoelimisha wananchi.

Akifungua mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa maafisa 282 wa mahakama wakiwemo majaji jijini Dodoma, amewataka wasajili kujitayarisha kutoa muhtasari wa hukumu husika kwa lugha nyepesi ili wananchi waweze kujifunza.

Ameongeza kuwa Ibara ya 113 A ya Katiba ya Tanzania, inawakumbusha Majaji, Mahakimu na Wasajili kutojiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa wanayo haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara ya 5 ya Katiba.

Amesema nafasi ya mahakama katika kuisaidia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwapa watanzania uchaguzi huru na wa haki, usio na vitendo vya jinai ni kwa Mahakama kutimiza wajibu wake wa kupokea, kusikiliza na kutoa maamuzi katika mashauri ya jinai yatakayojitokeza katika hatua mbali mbali za uchaguzi kwa haraka na kuacha Kuahirisha kusiko na lazima.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yanalenga kuwajengea uwezo maafisa wa Mahakama na kuwaandaa kutoa haki kwenye mashauri ya Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani.