Mahakama yatupilia mbali kesi ya kikatiba ya Mbowe

0
329

Mahakama Kuu ya Tanzania imetupilia mbali kesi ya kikatiba ya mwenyekiti wa Chama Cha Dokrasia na Maendeleo Chadema, Freeman Mbowe, ambaye alikuwa akipinga namna alivyowekwa kizuizini na kulazwa sakafuni kwa siku tano bila kufikishwa mahakamani.

Mahakama hiyo imetupilia mbali kesi hiyo baada ya majaji wanaoendesha shauri hilo kujiridhisha na hoja za jopo la mawakili Serikali lililoongozwa na Wakili Mwandamizi Hangi Chang’a kwamba kwa kuwa kuna kesi ya jinai dhidi Mbowe, basi alipaswa kuibua hoja zake katika mahakama hiyo kwanza kabla ya kufungua kesi ya kikatiba.

Mbowe alifungua kesi hiyo Julai 30, mwaka huu akilalamikia namna alivyotiwa mbaroni mkoani Mwanza nakuwekwa mahabusu ya polisi kwa siku tano bila kufikishwa mahakamani ndani ya saa 48 kama sheria inavyoelekeza.

Katika kesi hiyo namba 21 ya 2021, Mbowe alikuwa akipinga kufikishwa mahakamani bila kuwajulisha mawakili wake au ndugu zake na kabla ya kujulishwa kwa maandishi kuhusu mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.

Mbowe alifungua kesi dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon na Mwanasheria Mkuu wa Serikali AG. Aidha, alipinga kusomewa mashtaka ya ugaidi yanayomkabilia bila kuwa na wakili wala kupewa hati ya mashtaka na kudai kwamba utaratibu huo ulikiuka haki za kikatiba nakuomba mahakama itamke kuwa alinyimwa haki zake za msingi.

Majaji wa mahakama hiyo wamekubaliana na pingamizi la Serikali lililokuwa na hoja nne lililotaka kesi hiyo isisikilizwe kwa madai kuwa na kasoro nyingi za kisheria.

Aidha, mahakama imekubaliana na hoja moja tu ya pingamizi la Serikali iliyodai kuwa Mbowe hakutumia njia nyingine zilizopo kutafuta haki anazodai kabla ya kufungua kesi ya kikatiba.