Mahakama yataka kuharakishwa upelelezi kesi ya Sabaya

0
135

Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi imeutaka upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne kuharakisha upelelezi wa shauri hilo ili lisikilizwe mapema na washtakiwa wapate haki yao.
 
Sabaya amefikishwa mahakamani hapo leo pamoja na wenzake wanne ambao ni Silivester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey, wakikabiliwa na mashtaka saba ikiwemo kuendesha genge la uhalifu, kupokea rushwa, utakatishaji wa fedha pamoja na ukiukwaji wa mamlaka ya utumishi.

Hatua ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kutaka upande wa mashtaka kukamilisha haraka upelelezi inafuatia hoja iliyotolewa na upande wa utetezi kuhusu kuchelewa kwa upelelezi wa shauri hilo wakidai ni mara ya pili wamekuwa wakiambiwa upelelezi haujakamilika.

Tarehe 7 mwezi huu Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi iliahirisha shauri hilo baada ya upande wa mashataka kudai kuwa upelelezi haujakamilika.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 4 mwaka huu.