Mahakama yamwachia huru aliyekuwa bosi wa MSD

0
477

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya jijini Dar es Salaam imemwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu na aliyekuwa Mkurugenzi wa Logistiki, Byekwaso Tabura baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kutoa hati ya kuonesha nia ya kutokuendelea na mashitaka hayo.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Cassian Matembele baada ya upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon kuwasilisha hati ya kuonesha nia ya kutokuendelea na mashtaka hayo iliyosainiwa na DPP Mei 10, 2021.

Katika kesi hiyo, washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka matano ikiwemo la utakatishaji fedha haramu zaidi ya shilingi Bilioni 1.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka inadaiwa kati ya Julai 1, 2016 na Juni 30, 2019 katika maeneo tofauti ndani ya Dar es Salaam wakiwa watumishi wa umma waliongoza genge la uhalifu kwa ajili ya kujinufaisha wenyewe kinyume na sheria.

Wakili Wankyo amedai kuwa mshitakiwa Bwanakunu akiwa mtumishi wa umma alitumia madaraka yake vibaya kwa kuongeza mishahara na posho za wafanyakazi bila ruhusa ya Katibu Mkuu wa Utumishi na kuisababishia MSD hasara ya zaidi ya shilingi milioni 85.

Aidha wakili Wankyo amedai kuwa kati ya tarehe tajwa katika maeneo tofauti ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania washitakiwa hao kwa pamoja waliruhusu uhifadhi mbaya wa vifaa tiba na kusababisha vifaa hivyo kuharibika.

Katika shitaka la mwisho ilidaiwa kati ya tarehe hizo katika maeneo ya Keko, wilaya ya Temeke, mkoa wa Dar es Salaam washitakiwa hao kwa pamoja walijipatia fedha zaidi ya shilingi bilioni 1 zilizitokana na kuongoza genge la uhalifu.