Magofu yakwamisha ukusanyaji kodi ya ardhi

0
232

Uwepo wa magofu ya nyumba ambazo hazijajengwa wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, umekuwa ni changamoto kwa ofisi ya ardhi mkoa kushindwa kudai kodi ya ardhi kwa wahusika kutokana na kutopatikana kwa wakati.

Hayo yamesemwa na Afisa Ardhi wilayani Mwanga, Duncan Somi wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa licha ya kubandika notisi za madai ya kodi nyakati za mvua notisi hizo zinalowa na kubanduka kirahisi hivyo wahusika kushindwa kupata taarifa.

Duncan amesema iko sababu kwa serikali kuangalia upya sheria ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999 ambayo inamtaka mmiliki wa kiwanja kufanya maendelezo hivyo wengi wao wamekuwa wakijenga msingi na kutelekeza viwanja vyao.

Wananchi wilayani Mwanga wamesema magofu hayo yamekuwa sehemu za kushamiri kwa vitendo vya uhalifu na kuomba serikali isaidie kutoa tamko kama wamiliki wameshindwa kujenga wamilikishwe watu wengine.

Akizungumzia hali ya ulipaji wa kodi ya ardhi kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi mkoa Jeremiah Minja amewataka wadaiwa sugu kulipa tozo ya ardhi na sio kuongejea kufikishwa mahakamani.

Tayari Mashauri 54 ya kodi ya ardhi katika wilaya ya Mwanga na Same mkoani Kilimanjaro, yamefikishwa mahakama ya ardhi wilayani Same kutokana na wamiliki wake kuchelewa kulipa kodi za viwanja vyao.

Sauda Shimbo, Kilimanjaro