Jeshi la Magereza limeagizwa kujipanga upya kiutendaji na kutekeleza majukumu yake ya msingi.
Agizo hilo limetolewa Ikulu Chamwino mkoani Dodoma na Rais Samia Suluhu Hassan, mara baada ya kumuapisha Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza Mzee Ramadhan Nyamka pamoja na Majaji 21 wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Amesema kwa muda mrefu Jeshi la Magereza limeacha kutekeleza majukumu yake ya msingi, hivyo wakati umefika lijipange upya kiutendaji.
Amemtaka Kamishna Mkuu huyo wa Jeshi la Magereza kwenda kusimamia haki za mahabusu na wafungwa, kwani nao ni binadamu kama binadamu wengine.
Pia amemuagiza kwenda kujadiliana na maafisa wengine wa Jeshi hilo kuhusu changamoto zilizopo ili ziweze kushughulikiwa, hasa utawala bora.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema angependelea kuona Magereza yanakuwa sehemu ambayo watu wanapata elimu kuhusu mambo mbalimbali, ili wanapotoka wawe na mwanga katika kuendeleza maisha yao.