Mafia washindwa kukagua maendeleo kutokana na ukosefu wa magari

0
282


Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani inakabiliwa na ukosefu wa magari jambo ambalo linalosababisha Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo na wakuu wa idara kutembea kwa miguu kwenda kukagua  miradi ya maendeleo.


Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Mohamed Gomvu kwenye  kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Pwani kilichofanyika Mjini Kibaha.


Amesema halmashauri yake inakabiliwa na ukosefu wa magari jambo ambalo linasababisha watendaji kushindwa kwenda kusimamia miradi ya maendeleo.

Amesema hivi sasa wilaya nzima ina gari moja tu ambalo linatumiwa na Mkuu wa Wilaya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo Erick Mapunda amekiri kuwepo kwa tatizo hilo ambapo amesema pindi inapotokea dharura halmashuri hiyo hulazimika kutumia gari la  kanisa kufanyia shughuli zake.

Akizungumzia tatizo hilo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amemtaka Katibu Tawala wa Mkoa huo kushirikiana na afisa anayeshughukia serikali za mitaa kupeleka mara moja suala hilo Ofisi ya Rais Tamisemi ili liweze kushughulikiwa.