Madiwani Kinondoni wampongeza Sitta na Kagurumjuli

0
204

Baraza la madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni limewapongeza Mstahiki Meya Benjamini Sitta pamoja na Mkurugenzi Aron Kagurumjuli kwa kutekeleza miradi mikubwa katika kipindi cha miaka mitano ya utendaji kazi wao.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa kikao cha baraza la madiwani robo ya tatu ya mwaka ambapo wamesema kuwa katika kipindi ambacho wamekuwa madiwani wameshuhudia miradi mikubwa ambayo imetekelezwa ikiwa ni juhudi kubwa zinazofanywa na viongozi hao pamoja na watendaji.

Diwani wa Kata ya Mwananyamala, Songoro Mnyonge amesema kuwa kupitia Sitta na Kagurumjuli, Kinondoni imekuwa na mafanikio makubwa kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta ya elimu, Afya, Miundombinu, Masoko na Mazingira.

Mbali na miradi hiyo mikubwa, ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni stendi ya daladala ya mwenge, ofisi ya manispaa, uwanja wa mpira wa miguu, Soko la Magomeni, Tandale ambapo yote inatekelezwa na mapato ya ndani.

Diwani wa Kata ya Wazo, Joel Mwakalebela amesema kuwa kata yake imenufaika na fedha za halmashauri hiyo katika sekta ya elimu na afya kwani wananchi wake wamepata madarasa ya kisasa pamoja na vituo vya afya.

“ Ukipita kwenye mitaa huwezi kuona barabara ambazo hazipitiki, hata mvua ikinyesha ya namna gani, kwa hili kwakweli ninampongeza sana Mkurugenzi na timu yako,halmashauri hii inaviongozi wachapa kazi,” amesema amesema Diwani wa Viti Maalam Rose Mushi.

Kwaupande wake Mkurugenzi Kagurumjuli ameeleza kuwa mafanikio ya utekelezaji wa miradi hiyo umetokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina ofisi yake na Meya pamoja na watendaji.

Katika hatua nyingine baraza hizo limepitisha taarifa za kamati mbalimbali ambazo ni kamati ya Fedha na uongozi, Huduma za Uchumi, Kamati ya kudhibiti UKIMWI, Kamati ya Maadili pamoja na kamati ya mipango miji na mazingira.