Madaktari 9 wakutwa na hatia, wapewa adhabu

0
300

Baraza la Madaktari Tanganyika limewatia hatiani na kuwapa adhabu madaktari tisa kwa makosa ya ukiukwaji wa kanuni za maadili na utendaji wa kitaaluma.

Uamuzi huo ni matokeo ya kikao kilichokaa tarehe 22 hadi 26 Januari 2024 ambapo miongoni mwa adhabu zilizotolewa ni pamoja na kufutiwa usajili, kufungiwa leseni ya kutoa huduma kwa muda kati ya miezi sita hadi miaka miwili, kupewa onyo au karipio kali na pia walielekezwa kwenda kwenye mafunzo ya weledi, maadili ya kitaaluma na huduma kwa mteja ya wizara ya afya kwa muda wa miezi sita kwa gharama zao.

Mwenyekiti wa Baraza la Madaktari Tanganyika, Profesa David Ngassapa amesema wamebaini pia baada ya mapitio ya mashauri mbalimbali kuwa maeneo mengi ya misingi ya maadaili ya kitaaluma yameonekana kutokutiliwa maanani na wanataaluma kwenye kutoa huduma za afya kwa wagonjwa.

“Hivyo, Baraza linaelekeza kuzingatiwa kwa misingi ya maadili wakati wa kutoa huduma ikiwemo kujaza fomu za ridhaa ya huduma (informed consent) kwa mgonjwa, kumwelimisha mgonjwa madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa matibabu na kuwa kushindwa kufuata hayo, watakuwa wameenda kinyume na Sheria ya Udaktari, Udaktari wa Meno na Afya Shirikishi Sura Na. 152 pamoja na kanuni zake,” amesema.