Machinga wajitokeza kupata vitambulisho

0
1573

Zoezi la utoaji wa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo maarufu Machinga limeanza jijini Dar Es Salaam ambapo limeonyesha mafanikio.

Katika awamu ya kwanza wajasiriamali wadogo elfu moja wamepatiwa vitambulisho hivyo katika wilaya za Kinondoni na Ilala huku matarajio yakiwa ni kuwafikia wajasiriamali zaidi ya elfu kumi na tano kila wilaya.

Wilayani Kinondoni Mkuu wa wilaya hiyo Daniel Chongolo amezindua vitambulisho hivyo kwa kuwasajili na kugawa vitambulisho hivyo kwa wafanyabiashara wadogo mia tano huku akisema wilaya hiyo imepanga kutoa  vitambulisho elfu kumi na nane ili kuwafikia wamachinga walioko  katika Manispaa ya Kinondoni.

Chongolo ametoa tahadhari kwa wafanyabiashara wakubwa watakaobainika  kufanya udanganyifu kwa lengo la kukwepa kodi.

Zoezi hili pia limeendelea katika wilaya ya Ilala jijini Dar Es Salaam ambapo katika wilaya hizo za jiji la Dar Es Salaam wajasiriamali wameonekana kujitokeza kwa wingi kupata vitambulisho hivyo.

Hapo jana Desemba 10 mwaka huu Rais John Magufuli alikabidhi vitambulisho 670,000 vya wajasiriamali wadogo kwa wakuu wa mikoa ili vigawanywe kwa wajasiriamali lengo ikiwa ni kuwawezesha kufanya kazi zao bila bugudha na kuwezesha serikali kupata kodi.