Maboresho ya TBC yaleta mapinduzi ya upashanaji habari

0
174

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Abdallah Ulega amesema kwamba Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linaendelea kuimarisha usikivu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa studio za televisheni Mikocheni Dar es Salaam.

Ulega ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilipopokea taarifa kuhusu mradi wa ujenzi wa studio hiyo pamoja na ujenzi wa redio ya jamii Makao Makuu ya nchi, Dodoma.

“Taarifa inayowasilishwa kwenu leo itawezesha kupatikana uelewa wa hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi hii na mtakapoitembelea mtapata fursa ya kuona hali halisi ya utekelezaji,” amesema Ulega.

Akiwasilisha taarifa hiyo Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba ameeleza kuwa katika bajeti ya miradi ya maendeleo ya takribani shilingi milioni 900 iliyoidhinishwa, pamoja na shilingi bilioni 1 kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) zilitekeleza uboreshaji wa mfumo wa umeme na ufungaji wa ‘AVR na UPS,’ ununuzi na ufungaji wa mitambo na vifaa vya redio pamoja na ukarabati wa jengo la studio.

“Baada ya uboreshaji kupitia fedha hizo manufaa mbalimbali yamepatikana ikiwemo kuaandaa na kurusha vipindi vya redio na televisheni kutokea Dodoma, matangazo ya televisheni ya kipindi cha ARIDHIO na Jambo Tanzania yamekuwa yakirushwa kutokea Dodoma,” Amesema Dkt. Rioba.

Ameongeza kuwa manufaa mengine yaliyotokana na mradi huo ni kurushwa mbashara vipindi vinavyohitaji ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kitaifa kutoka kwa viongozi wa Serikali muda wote inapohitajika kufanya hivyo pamoja na redio jamii kuhusika kurusha habari za kikanda hivyo kuleta uelewa kwa wananchi kuhusiana na kazi wanazofanya.