Mabinti waaswa kutumia vyema mitandao ya kijamii

0
386

Wasanii wamekuwa kioo cha jamii kwa muda mrefu na sasa mitandao ya kijamii imeibuka na kuchukua nafasi hiyo kwa kuwa mwalimu na sehemu ya vijana wengi kutafuta ‘role model’.

Hayo yamebainishwa jana katika Kongamano la kuelekea Siku ya Wanawake Duniani itayoadhimishwa kimataifa Machi 8.

Vincensia Fuko, Wakili wa Kujitegemea na Mkurugenzi wa Shirika la Mediaspace Tanzania amewataka mabinti kuitumia vyema mitandao ya kijamii na kuchagua aina ya mambo ya kuweka kwenye kurasa zao na kutafakari matokeo yake kwao na jamii kwa ujumla.

“Vijana wote wa kike na wa kiume tutumie mitandao ya kijamii vizuri. Hii mitandao ya kijamii sasa hivi ndio kioo,” amesisitiza Fuko.

Katika kipindi cha hivi karibuni imeonekana kuwa mitandao ya kijamii imekuwa ikitumika kumdhalilisha mwanamke jambo ambalo hupelekea athari za kisaikolojia.

Akizungumza katika kongamano hilo lililofanyika Millenium Towers, Dar es Salaam, Dkt. Lusajo Kajula, Msaikolojia Tiba ameeleza kuwa afya ya akili inaweza kuathiri maisha ya kila siku ya mtu kuanzia mahusiano na wakati mwingine kupelekea maumivu ya mwili.

Mtu kuwa na afya bora ya akili sio kutokuugua ugonjwa wa akili bali ni “kuwa na ustawi kwa ujumla wa mawazo, tabia hadi hisia.”

Wadhamini wa kongamano hilo lililojumuisha wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo vikuu wamesisitiza mabinti kuchanja na kutambua umuhimu wa chanjo si kwa ajili ya afya zao pekee bali pia kuwalinda wale wanaowazunguka.