Mabalozi watembelea miradi Zanzibar

0
201

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo yaNje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ramadhani Mwinyi, ametoa wito kwa Mabalozi wanaoiwakilisha  Tanzania katika nchi mbalimbali duniani,  kutumia fursa walizoziona katika miradi mbalimbali ya maendeleo waliyoitembelea hapa nchini kuitangaza Tanzania Kimataifa.

Balozi Mwinyi ametoa wito huo Kisiwani Unguja, wakati wa ziara ya Mabalozi hao ambao wametembelea miradi mikubwa kadhaa ya maendeleo inayotekelezewa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Wakiwa katika jengo la abiria linaloendelea kujengwa katika  uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, baadhi ya Mabalozi hao wamesema kuwa,  kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza idadi ya Watalii wanaoitembelea Tanzania.

Wengine wamesema kuwa ziara yao ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, itaongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Kwa upande wake Mkurugenzi  wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Dkt Miraji Ukuti Ussi,  amewaeleza Mabalozi hao wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali Duniani kuwa,  kila mwaka kumekuwa na ongezeko la asilimia Ishirini ya Watalii wanaoitembelea Zanzibar.

Miradi iliyotembelewa na Mabalozi hao huko Zanzibar ni pamoja na ujenzi wa maduka ya Michenzani, ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, mradi wa nyumba katika mji wa kisasa  wa Fumba, mradi wa ujenzi wa barabara katika mkoa wa Kaskazini Unguja na eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya mafuta Mangapwani.